Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kohsari, Naibu wa Kimataifa wa Hawza, katika mkutano wa kuimarisha ushirikiano na kutoa pongezi kwa uwepo na nafasi muhimu ya wanachuo wa Hawza na wanazuoni katika mchakato wa kutoa huduma kwa wananchi wa Lebanon wenye msimamo imara na wenye kujivunia, ambao ulifanyika kwa lengo la kuthamini juhudi za wanachuo na wanazuoni katika kuliunga mkono taifa tukufu la Lebanon, kuchunguza uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za moja kwa moja katika medani ya Muqawama, na kufafanua uwezo mpana wa Hawza za Elimu za Kiislamu katika medani ya kimataifa, amewasilisha salamu, pongezi na shukrani za Marajii Wakuu wa Taqlidi, Baraza Kuu la Hawza na Ayatullah Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, kwa juhudi za mchana na usiku pamoja na jitihada za dhati zinazofanywa na wanachuo wa kijihadi katika kuwahudumia wananchi wa Lebanon.
Naibu wa Kimataifa wa Hawza, akizungumzia mazingira magumu na kipindi cha dhiki na hofu kinacholikabili taifa la Lebanon, ameutaja uwepo wa wanachuo na wanazuoni wa Iran pamoja na wananchi wa nchi hiyo kuwa ni mfano wenye mafanikio na wenye thamani wa “ushiriki wa kimataifa”, na kusema: “Leo, mifumo ya uhubiri na uwepo katika medani ya kimataifa imepitia mabadiliko makubwa ikilinganishwa na zamani. Hatua yenu, enyi wanachuo wa kijihadi, ilikuwa mfano wa wazi wa kusimama pamoja na taifa la Lebanon; mfano ulioonesha kwamba Hawza, hata zaidi ya zana za kimapokeo na uhubiri unaotegemea kujua lugha, zinaweza kuwa na uwepo wenye taathira, unaoleta mabadiliko na wenye mtazamo wa kistaarabu katika medani.”
Akiendelea kusisitiza kuhusu mabadiliko ya haraka yanayotokea duniani kwa manufaa ya mkondo wa haki na fikra ya Muqawama, aliongeza: “Leo tunakabiliwa na wimbi kubwa la watu wanaovutiwa na maarifa ya Ahlul-Bayt (as) na fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali duniani. Hali hii inahitaji wanachuo na wanazuoni kuchukua nafasi kubwa zaidi, kuongoai na kuwa na uwepo hai katika medani za kimataifa, ili waweze kuwa waongozaji katika njia ya harakati hii yenye nuru.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kohsari pia, akizungumzia mambo nyeti na mazingira maalumu ya kazi za kimataifa, hususan katika nyanja za vyombo vya habari na usalama, amesisitiza umuhimu wa kuinua kiwango cha uwezo wa wahitimu wa Hawza, kufanya utafiti wa kina kuhusu maarifa ya Qur’ani, fikra za Shahidi Murtadha Mutahhari, pamoja na kueleza kwa usahihi mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Akiainisha mahusiano mapana ya Hawza na taasisi, Hawza, wanazuoni wa Ahlus-Sunna na viongozi wa dini mbalimbali nchini Lebanon, amesisitiza: “Kuhifadhi na kuimarisha mahusiano ya kimkakati na nchi kama Lebanon na Iraq ni miongoni mwa vipaumbele vya msingi, na uwezo ulioanzishwa kupitia taasisi na makundi ya kijihadi unaweza kuwa nyongeza na nguzo ya kuimarisha njia hii.”
Uwepo wa Moja kwa Moja katika Medani; Mchakato wa Kujenga Utambulisho na Malezi kwa Kizazi Kipya cha Hawza
Katika kuendelea kwa mkutano huo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ishaqi, Mkuu wa Kambi ya Wananchi ya Lebanon na Mkuu wa Dawati la Hawza la Lebanon, pamoja na kundi la wanachuo na wanaharakati wa kijihadi waliokuwepo katika mkutano huo, waliwasilisha ripoti, kueleza uzoefu wao na kufafanua nyanja mbalimbali za uwepo wa wanachuo katika mchakato wa kutoa misaada kwa wananchi wa Lebanon.
Kwa mujibu wa hoja zilizojadiliwa katika mkutano huo, miongoni mwa baraka muhimu za uwepo wa wanachuo katika medani za moja kwa moja kama Lebanon, Syria na hata maeneo yenye huduma duni ndani ya nchi, ni athari yake kubwa katika malezi. Kukabiliana moja kwa moja na hali halisi ya medani ya Muqawama na masuala ya ulimwengu wa Kiislamu kuwatoa wanachuo katika mazingira ya fikra za kinadharia pekee na kuwafungulia upeo mpya katika njia ya kuwahudumia wengine.
Katika mkutano huo pia ilisisitizwa kwamba; kutambulisha njia mpya kama vile “mhubiri wa kimataifa,” “mshiriki wa kijamii,” na “mwanaharakati wa kijihadi katika medani ya Muqawama” kunaweza kuweka mbele ya kizazi kipya cha Hawza picha ya mustakabali ulio wazi, wenye nguvu na wenye kuhamasisha kuhusu majukumu na ujumbe wa kuwa mwanafunzi wa Hawza.
Kupanua Mfumo wa Msaada wa Wananchi na Kuunganisha Uwezo wa Hawza
Miongoni mwa mambo mengine muhimu yaliyozingatiwa katika mkutano huo ni kuchunguza uzoefu wenye mafanikio wa “mfumo wa safari za wananchi za kutoa huduma” na kuunganisha uwezo wa maeneo mbalimbali ndani ya nchi na medani ya kimataifa.
Uzoefu wa uwepo wa wanachuo wa kijihadi nchini Lebanon umeonesha kwamba ushiriki wa kimataifa wa Hawza unaweza kuibua wimbi la mshikamano na kuijenga jumuiya ya ushiriki ndani ya nchi; kiasi kwamba uwepo wa wanachuo katika eneo hilo umesababisha misikiti, Hay’ah na taasisi za kiutamaduni katika miji na maeneo mbalimbali kuanza kufanya kazi katika kutoa taarifa na kukusanya misaada mikubwa ya wananchi kwa ajili ya Muqawama. Katika mchakato huu, mwanafunzi wa Hawza anatekeleza nafasi ya kiungo kinachounganisha uwezo wa wananchi na medani ya kiutendaji ya Muqawama.
Aidha, katika mkutano huo ilisisitizwa kuhusu utofauti wa programu zilizotekelezwa nchini Lebanon kulingana na mahitaji na mazingira ya kila eneo. Miongoni mwa hatua hizo ni kutoa huduma za kijamii na misaada kwa watu waliokimbia makazi yao, kuendesha programu za malezi na utamaduni kwa watoto, kuandaa kozi za kuwafundisha walezi na wakufunzi, kufanya tafiti za kijamii, pamoja na kuendesha programu za vyombo vya habari, ambazo zimefanyika kwa lengo la kuwaandaa wataalamu wa wenyeji na kujenga uwezo endelevu.
Mwisho wa mkutano huo, kwa kutolewa na kukabidhiwa vyeti vya pongezi na zawadi za kumbukumbu, wanachuo na wanazuoni waliheshimiwa na kutambuliwa kwa nafasi yao muhimu, juhudi zao za kijihadi na uwepo wao wenye thamani katika mchakato wa kuwahudumia wananchi wa Lebanon wenye msimamo imara na wenye kujivunia.
Maoni yako